Nafasi Ya Matangazo

April 16, 2024

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendelea ya Makazi, Mhe. Jerry Slaa amewataka watumishi wa ardhi nchini, kuwa waadilifu na hofu ya Mungu kwa kutenda haki wakati wanaposuluhisha migogoro ya ardhi.

Mhe. Slaa ameyasema hayo mapema leo Aprili 15, 2024, wakati akifungua kliniki ya ardhi Mkoa wa Mbeya itakayofanyika hadi Aprili 17, 2024, Jijini hapa. Amewakumbusha watumishi wa Ardhi kutenda haki kwa wananchi na kuwa na hofu ya Mungu, kwani kushindwa kutatua jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wao ni kumkosea Mungu.

Aidha Mhe. Slaa ameendelea kusisitiza kufanya kazi kwa kumsaidia Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini pia kufanya kazi kwa ajili ya wananchi katika upande wa ardhi ili kupunguza kero na migogoro isiyokuwa na ulazima katika jamii.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera amempongeza Mhe. Slaa kwa kuitumikia vyema sekta ya ardhi kwa kutatua migogoro mbalimbali nchini ikiwa ni moja ya jitihada za kumsaidia Mhe. Rais kwa vitendo.

Katika Kliniki hiyo ya Ardhi inayofanyika katika ukumbi wa Mkapa, wakazi wa Mkoa wa Mbeya watapata huduma ya kusikilizwa na kutatuliwa changamoto mbalimbali zinazohusu ardhi.

Posted by MROKI On Tuesday, April 16, 2024 No comments

April 15, 2024


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga akiangalia utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere kupitia kifaa cha uhalisia pepe (VR) katika Maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga akizungumza na Wataalam mbalimbali kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati walioshiriki Maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga akipata maelezo kuhusu utekelezaji wa Sekta ya Nishati katika Wiki ya Maonesho ya Nishati inayoendelea katika Viwanja  vya Bunge jijini Dodoma. Anayetoa maelezo ni mtaalam kutoka Wizara ya Nishati Joyce Msangi.
************
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ametoa wito kwa wananchi na Wabunge nchini kutembelea Maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma ili kufahamu masuala mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Naibu Waziri Kapinga ametoa wito huo tarehe 15 Aprili, 2024  baada ya kutembelea mabanda ya Maonesho hayo na kujionea jinsi Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Wadau wake walivyojipanga tayari kwa kuhudumia Wabunge na Wananchi watakaotembelea maonesho husika.

“ Nawakaribisha Wananchi na Wabunge kwenye Wiki hii muhimu sana ya Nishati, ambapo tunaonesha kazi mbalimbali zinazofanywa na Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zake, tunatatua kero mbalimbali zinazowasilishwa na pia Wabunge na Wananchi watajionea utekelezaji wa miradi katika wilaya zote, majimbo yote na mikoa yote Tanzania.”  Amesema Mhe. Kapinga

Ameongeza kuwa, katika Maonesho hayo Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Nishati pamoja na kampuni zake tanzu zimeshiriki.

Mhe. Kapinga amesema kuwa, katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kazi kubwa imefanyika katika Sekta ya Nishati akitolea mfano utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao umeshaanza kuzalisha umeme, miradi ya usambazaji umeme mijini, vijijini na vitongojini, nishati safi ya kupikia pamoja na sekta ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia.

Aidha, kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Mhe. Kapinga amemshukuru Spika wa Bunge, Mhe. Dkt.Tulia Ackson kwa kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Nishati ambao umewezesha Wiki ya Nishati kufanyika kwa umahiri mkubwa.

Maonesho ya Wiki ya Nishati yaliyoanza leo yatahitimishwa tarehe 19 Aprili 2024 ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko atayafungua rasmi tarehe 16 Aprili 2024.



Posted by MROKI On Monday, April 15, 2024 No comments

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, akiwataka wakaguzi wa ndani barani Afrika kutumia utaalam wao wa ukaguzi kuzisaidia nchi zao kutatua chamgamoto, wakati wa Mkutano wa 10 wa Wakaguzi wa Ndani Barani Afrika, unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Mkaguzi Mkuu wa Ndani (IAG), Bw. Benjamini Magai, akizungumzia umuhimu wa Ukaguzi kwa maendeleo, wakati wa Mkutano wa 10 wa wakaguzi wa ndani barani Afrika, unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, akiongozwa na Rais wa Taasisi ya Ukaguzi Tanzania, Dkt. Zelia Njeza (Kulia) na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Afrika, Bi. Ruth Mutebe, wakati wakiingia kwenye mkutano wa Viongozi wa Ukaguzi wa Ndani kwenye Mkutano wa 10 wa Wakaguzi wa Ndani Afrika, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, akizungumza jambo na Rais wa Taasisi ya Ukaguzi Tanzania, Dkt. Zelia Njeza (Kushoto) wakati wa mkutano wa 10 wa Wakaguzi wa Ndani Afrika, unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, akiteta jambo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Ukaguzi Afrika, Bi. Ruth Mutebe (Kushoto) wakati wa mkutano wa 10 wa Wakaguzi wa Ndani Afrika, unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum (wa pili kushoto), akiwa katika mkutano na Bodi ya Wakurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani wa Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani Duniani (IIA Grobal) wakati wa Mkutano wa 10 wa Wakaguzi wa Ndani Afrika, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum (wa tano kushoto), Mwenyekiti wa Taasisi ya Ukaguzi Afrika, Bi. Ruth Mutebe (wa sita kulia), Rais wa Taasisi ya Ukaguzi Tanzania, Dkt. Zelia Njeza (wa sita kushoto), Mkaguzi Mkuu wa Ndani (IAG), Bw. Benjamini Magai (wa nne kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Bodi ya Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani Duniani na wajumbe wengine, wakati wa mkutano wa 10 wa wakaguzi wa ndani Afrika, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

************
Na. Peter Haule, WF, Arusha
Wakaguzi wa Ndani barani Afrika wametakiwa kubadilishana uzoefu na kutumia teknolojia katika kutatua changamoto mbalimbali katika taaluma yao na kuhakikisha wanasaidia taasisi na Serikali zao kuboresha ufanyaji kazi ili kuchochea maendeleo.
 
Hayo yameelezwa jijini Arusha na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, wakati wa Mkutano wa 10 wa Wakaguzi wa Ndani Barani Afrika, ulioanza kwa mikutano midogo inayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
 
Dkt. Mkuya alisema kuwa mkutano huo umewakutanisha wakaguzi kutoka nchi 27 za Afrika na kwamba mkutano huo ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu ambapo wageni watajifunza Tanzania na wageni watajifunza kwa wenzao kwa kuwa mazingira ya ukaguzi yamebadilika kutokana na kuimarika kwa teknolojia duniani.
 
‘’Tumezoea kuona ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu (CAG) lakini kuna wakaguzi wa ndani ambao wanafanya kazi kila siku ambao husimamia taratibu za matumizi ya fedha, utawala na mifumo hivyo mawanda yao ni mapana katika masuala ya ukaguzi hivyo mkutano huu ni muhimu sana kwa nchi”, alisema Dkt. Mkuya.
 
Alisema Kada ya ukaguzi wa ndani watu wengi hawaielewi hivyo mkutano huo utasaidia kujua mamlaka ya mkaguzi, maadili na taratibu za kufuata ili kuwa na ufanisi katika utendaji kazi.
 
Aidha, Dkt. Mkuya alisema mkutano huo utafuatiwa na mkutano Mkuu utakaofunguliwa Aprili 17 mwaka huu na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
 
Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya Ukaguzi Tanzania (IIA Tanzania), Dkt. Zelia Njeza, alisema kuwa mkutano wa 10 wa Wakaguzi wa Ndani Afrika umehudhuriwa na Bodi ya Wakurugenzi wa Ukaguzi Duniani (IIA Global) ambao kabla ya mkutano huo wa 10 walikuwa na Kikao chao cha Bodi, jijini Arusha.
 
Alisema kuwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya IIA Grobal kuwa na mkutano wao wa Bodi Afrika hivyo Tanzania inajivunia kupata ujio huo ambao unafaida kwa kada ya ukaguzi lakini pia katika sekta ya utalii.
 
Dkt. Zelia alisema kuwa mkutano huo unategemea kuwa na washiriki zaidi ya 1,000 na kati yao washiriki 300 ni wageni kutoka nchi za Afrika na nje ya Afrika.
 
Alisema mkutano Mkuu wa Wakaguzi utafanyika kwa siku tano ambapo umeanza na mkutano wa Jukwaa la Viongozi kutoka taasisi za umma na binafsi ambao wengi ni Wakurugenzi wa Bodi, Taasisi na Wakuu wa Vitengo vya Ukaguzi wa Ndani.
 
Dkt. Zelia alisema kuwa, mkutano huo utasaidia kubadilishana mawazo na kuwa sauti ya pamoja ya kada ya wakaguzi katika kutatua changamoto mbalimbali na kuzisaidia nchi za Afrika kuongeza kasi ya maendeleo.
 
Aidha alizitaja mada zitakazowasilishwa kuwa ni pamoja na mazingira, utawala bora na uadilifu, ambapo alisema mada hizo zitaenda sambamba na majadiliano yatakayoondoa kufanya kazi kwa mazoea na kuwa na sauti moja ya wakaguzi kwa kufanya kazi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
 
Mkutano kama huo wa Wakaguzi Afrika ulifanyika nchini Zambia mwaka 2022 na katika mkutano huo Tanzania ilifanikiwa kushinda kuwa mwenyeji wa mkutano wa 10 baada ya kushindanishwa na nchi nyingine barani Afrika.
Posted by MROKI On Monday, April 15, 2024 No comments

 

Ameyasema hayo leo jioni (Jumatatu, Aprili 15, 2024) Bungeni, jijini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2024/2025.

 

“Serikali imeendelea kutekeleza sera mbalimbali za uwezeshaji wa makundi maalum ya wanawake, vijana na wenye ulemavu. Lengo likiwa ni kuhakikisha makundi haya yanashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hapa nchini.”

 

Amesema katika kutekeleza sera ya ushirikishwaji wa Watanzania kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji nchini, wanawake na vijana wameendelea kunufaika kupitia miradi ya kimkakati na uwekezaji ambapo katika mwaka 2023/2024, Watanzania 162,968 wamenufaika na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

 

“Serikali imeendelea kuratibu masuala ya uzalishaji wa fursa za ajira nchini kwa kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji na kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, fursa za ajira 2,489,136 zimezalishwa sawa na wastani wa ajira mpya 829,712 kwa mwaka,” amesema.

 

Kuhusu vijana, Waziri Mku amesema Serikali imeendelea kuwawezesha vijana ili waweze kujiari, kushiriki kwenye shughuli za maendeleo na kuchangia katika Pato la Taifa. “Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, shilingi bilioni 3.19 kimetolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambazo zilitumika kutoa mikopo ili kuwezesha miradi 148 katika sekta za kilimo, viwanda na biashara katika halmashauri 62.”

 

Amesema Serikali imetoa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi, kurasimisha na kuendeleza biashara kwa vijana katika maeneo mbalimbali nchini. Ambapo hivi karibuni, Ofisi ya Rais - TAMISEMI itatoa taarifa ya mfumo utakaotumika kutoa mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri nchini.

Katika hatua nyingine, akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira, Waziri Mkuu amesema kuwa athari za uharibifu wa mazingira ni mbaya kwa kuwa huathiri masuala ya kijamii na kiuchumi.

“Mara kadhaa tumeshuhudia vifo vya mifugo kutokana na ukame na uhaba wa maji vilivyotokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababishwa na uharibifu wa mazingira. Vilevile, mvua nyingi kupita kiasi zimeendelea kusababisha athari kubwa nchini ikiwemo mafuriko, vifo na uharibifu wa miundombinu mbalimbali.”

Kutokana na umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, Waziri Mkuu ametoa maagizo matano kwa viongozi nchini ambayo yanawataka viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji hadi mikoa wasimamie kikamilifu uhifadhi wa mazingira na suala hili liwe ajenda ya kudumu katika vikao vyao.

Pia amewataka viongozi wa Mikoa na Wilaya wasimamie utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu athari za kuchoma misitu ovyo, kufuga bila kuangalia uwezo wa maeneo ya kulishia, kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kuondokana na tabia ya kukata miti ovyo.

Aidha, amezitaka Halmashauri zote nchini zisimamie kikamilifu sheria ndogo za uhifadhi wa mazingira na kuwachukulia hatua watu wote wanaofanya uharibifu wa mazingira

“TFS na Halmashauri ziandae vitalu vya miti inayoendana na ikolojia ya maeneo yao, kuigawa kwa wananchi, kuhakikisha inapandwa na kukua. Hatua hii iende sambamba na kusimamia upandaji wa miti kwa kila kaya. Vilevile,TANROADS na TATURA wahakikishe wakandarasi wanapanda miti pembeni mwa kila mradi wa ujenzi wa barabara.

Pia amewataka wananchi waendelee kushirikiana na Serikali katika uhifadhi wa mazingira ili kuepusha madhara yatokanayo na uharibifu wa mazingira katika nchi yetu.

Kwa mwaka 2024/2025, Bunge limeidhinisha sh. 350,988,412,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 146,393,990,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 204,594,422,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.

 

Vilevile, Bunge limeidhinisha sh. 181,805,233,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 172,124,423,000/- ni za matumizi ya kawaida na sh. 9,680,810,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipongezwa na Waziri wa Nchi-Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mheshimiwa Jenista Mhagama, pamoja na Mawaziri wengine baada ya kuhitimisha hoja ya bajeti Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake, na mfuko wa Bunge kwa mwaka 2024/2025, bungeni jijini Dodoma, Aprili 15, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipongezwa na Mbunge wa Viti Maalum Ester Matiko, mara baada ya kuhitimisha hoja ya bajeti Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake, na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2024/2025 bungeni jijini Dodoma, Aprili 15, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa Katika picha ya pamoja na Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi na Idara wa Ofisi ya Waziri Mkuu mara baada ya kuhitimisha hoja ya bajeti Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake, na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2024/2025 bungeni jijini Dodoma, Aprili 15, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Posted by MROKI On Monday, April 15, 2024 No comments


🔴
Nia ni 
kuwawezesha wananchi kuelewa mwenendo wa mashauri

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mahakama zimeanza kutumia mfumo unaonasa sauti na kuzibadilisha kwenda kwenye maandishi huku ukitafsiri lugha za Kiingereza na Kiswahili.

 

“Hii ni hatua kubwa sana kwani mfumo huo unarekodi sauti na kupeleka kwenye maandishi. Vilevile, unaweza kutafsiri lugha ya Kiswahili au Kiingereza kulingana na uhitaji,” amesema na kuongeza: “Kanuni za Mahakama zimeanza kutafsiriwa sambamba na uandaaji wa mihutasari ya hukumu kwa Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuelewa mwenendo wa mashauri.”

 

Ametoa kauli hiyo leo jioni (Jumatatu, Aprili 15, 2024) Bungeni, jijini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2024/2025.

 

Akielezea mambo yaliyofanyika ndani ya miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita, Waziri Mkuu amesema mbali ya matumizi ya Kiswahili mahakamani, Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na  teknolojia kutokana na  mapinduzi ya nne ya viwanda duniani.

 

“Jitihada hizo zimeanza kuleta mafanikio katika utendaji wa Serikali kwa kuunganisha Serikali yote (Wizara, Idara, Wakala na Taasisi zake) ziweze kusomana kimfumo. Tumeanza kupata mafanikio mfano: Mahakama ya Tanzania, ambapo mifumo mbalimbali ya TEHAMA imejengwa ili kurahisisha na kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.”  

 

Waziri Mkuu ameitaja mifumo hiyo kuwa ni pamoja na  Mfumo wa Usajili, Uendeshaji na Usimamizi wa Mashauri kwa ajili ya kurahisisha, kuharakisha na kuokoa muda wa mwenendo wa mashauri mahakamani.

 

“Mfumo mwingine ni wa unukuzi na kutafsiri mienendo ya mashauri Mahakamani kwa lengo la kuwa suluhu ya kudumu ili kuwawezesha Waheshimiwa Majaji na Mahakimu kuondokana na adha ya kuandika kwa mkono mwenendo wa mashauri,” ameongeza.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha mfumo wa utoaji haki unaboreshwa, Januari 31, 2023, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda Tume maalum aliyoipa jukumu la kushauri namna njema ya kuboresha mfumo na utendaji kazi wa taasisi zinazohusika na haki jinai.

Akielezea maboresho ya mfumo wa utoaji haki na taasisi za hakijinai, Waziri Mkuu amesema: “Tume hiyo, ilipokea maoni kutoka kwa wananchi na wadau wengine wa hakijinai na kutoa mapendekezo ya maboresho yanayohitajika kufanyika. Tangu Tume ilipowasilisha mapendekezo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za maboresho ya mfumo wa utoaji wa hakijinai ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa taasisi za hakijinai.”

Amesema Serikali inaendelea kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki zao kwa wakati na waweze kuendelea kufanya shughuli za maendeleo yao binafsi na Taifa zima kwa ujumla.

“Hii ndiyo dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukidhi kiu na matarajio ya wananchi ya utoaji wa hakijinai kuanzia hatua za uchunguzi, ukamataji wa watuhumiwa hadi utoaji wa hukumu yenye haki mahakamani,” amesisitiza. 1 

Kwa mwaka 2024/2025, Bunge limeidhinisha sh. 350,988,412,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 146,393,990,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 204,594,422,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.

 

Vilevile, Bunge limeidhinisha sh. 181,805,233,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 172,124,423,000/- ni za matumizi ya kawaida na sh. 9,680,810,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Posted by MROKI On Monday, April 15, 2024 No comments





Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuhakikisha linapeleka huduma ya umeme kwenye maeneo ya miradi ya maendeleo ili kuharahisisha huduma kwa wananchi.

Dkt. Biteko amesema hayo akiwa Loliondo, wilayani Ngorongoro baada ya kuzindua minara ya kurushia matangazo ya TBC Taifa na Bongo fm.

Amesema miradi inatekelezwa na itakuwa ya mafankio endapo Taasisi husika zitakaa pamoja na kuandaa maeneo yanayohitaji utekelezaji katika hatua mbalimbali.

  "TANESCO, REA, UCSAF na TBC  zikae pamoja wakati wa uandaaji wa miradi husika ili miradi iwe inatekelezeka kwa tija, ufanisi na kwa haraka".

Pia,  ameiagiza TARURA kuhakikisha huduma ya barabara zinafikika katika maeneo ilipojengwa mitambo ya redio ambayo ipo sehemu kubwa ya milimani nchini ili kuwa na miundombinu imara.

Pia, ameipongeza TBC kwa maboresho makubwa ya miundombinu ya utangazaji, maboresho ya studio, mitambo na vifaa vya kisasa, ubora wa maudhui pamoja na ubunifu katika kuwahabarisha Watanzania.

"Mimi nafuatilia habari za TBC nafahamu chaneli ya TBC mahsusi kwa ajili kutangaza utalii (Safari Chaneli), redio ya vijana ya Bongo FM na televisheni ya vijana ya TBC2. TBC imekuwa na kampeni maalum kama vile: 27 ya Kijani kupitia Jambo Tanzania, Elimu kwa Umma kuhusu Tume ya Haki Jinai, vipindi vya kimkakati vyenye lengo la kukuza uzalendo (Mizani, jioni njema, jamvi la machweo na Lulu za Kiswahili)," amesema Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewataka wananchi ambao mitambo hiyo imezinduliwa katika wilaya za Ngorongoro, Arusha, Uvinza  Kigoma, Makete - Njombe na Kyela  Mbeya, kuhakikisha wanaitunza mitambo hiyo kwa maslahi ya wananchi wote.

"Nimetaarifiwa kuwa usikivu wa redio za TBC katika kipindi cha miaka mitatu (2020/2021 – 2022/2023) ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umeongezeka kutoka asilimia 74 (2020/2021) hadi kufikia asilimia 85 (2022/2023) na utafikia asilimia 92 baada ya kukamilika miradi inayoendelea kwa Mwaka huu wa Fedha 2023/2024," amesema Dkt. Biteko.

Kuhusu uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa amewasihi watanzania kufanya  maamuzi sahihi kwa kuchagua viongozi watakaoleta maendeleo kwani Wananchi wanachotaka ni maendeleo na sio siasa.

"Tujitahidi kusikiliza vizuri sera za wagombea watakaoamua kuwania na tuamue kwa utulivu na kwa kumshirikisha Mwenye Mungu ili lengo kuu la kuwa na viongozi lifikiwe," ameongeza Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye amesema TBC inaendelea kuboresha miundombinu ya utangazaji ili kuwahabarisha Watanzania.

Aidha, amewataka Watanzania kusimama na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Rais amegusa maisha ya Watanzania kwa kuleta fedha na kujenga ncjo, kuboresha miundombinu mbalimbali hapa nchini.
Posted by MROKI On Monday, April 15, 2024 No comments
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo tarehe 15 Aprili, 2024 amezindua vituo vya kurushia matangazo vya TBC Taifa na Bongo FM.

Uzinduzi huo umefanyika Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kwa niaba ya vituo vingine vya Uvinza, Kyela, Makete na Mbinga.

Viongozi wa Serikali na wadau mbalimbali wa Sekta ya Habari na Mawasiliano wamehudhuria.








Posted by MROKI On Monday, April 15, 2024 No comments








Mbunge wa Kigamboni Dkt Faustine Ndugulile Mb amekipongeza Chama cha Mpira wa miguu Kigamboni (KDFA) kwa kuandaa mashindano mazuri ya veterans,
 "Kwanza, nianze kuwapongeza KDFA kwa kuanzisha mashindano haya ya veteran cup ambayo leo 14, Aprili 2024 yamefika tamati. Mashindano yaliyojumuisha timu kumi na moja (11) kutoka wilaya yetu ya kigamboni kiukweli yalikuwa mazuri sana na fainali ya leo kiukweli imetupatia burudani nzuri."
"Ndugu
zangu niwaombe tuendelee kufanya mazoezi kwa ajili ya kufahamiana, kujenga urafiki na kuimarisha afya zetu".
Mashindano haya yamekutanisha baadhi ya wachezaji wa zamani wa timu za Simba na Yanga.

Fainali ilikutanisha Gezaulole veterans na kibada veterans, ambapo mchezo ulimalizika dakika tisini 90 bila kufungana na Gezaulole veterans kuibuka bigwa wa mashindano kwa kushinda mikwaju ya penati 5 na nne kwa  Kibada veterans.

Aidha, Dkt Ndugulile amemwagiza mwakilishi wa  Afisa utamaduni, Sanaa na michezo wa wilaya ya Kigamboni Bi Twidike Ntwima kuhakikisha viwanja vyote vya michezo vifuatiliwe na vitambuliwe ili vikabidhiwe Kwa timu za maeneo husika kwa matumizi, kuvitunza na kuviendeleza ili kuepuka uvamizi wa viwanja vya michezo.
Posted by MROKI On Monday, April 15, 2024 No comments

April 14, 2024

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa zawadi maalum na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.Dkt. Selemani Jafo, baada ya kutembelea baanda la maonesho la Ofisi hiyo wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganika na Zanzibar, yanayofanyika katika viwanja vya Maonesho vya Nyamazi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 14-4-2024.(Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akikagua banda la Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Viwanja vya Maonesho ya Biashara Nyamanzi Mkoa wa Mjini Magharibi leo Aprili 14, 2024. Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Bw. Abdallah Hassan Mitawi.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Viongozi mbalimbali wa Serikali alipowasili katika viwanja vya Nyamazi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, kwa ajili ya Uzinduzi Rasmin wa  Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa  Tanganyika na Zanzibar, uliofanyika leo 14-4-2024 katika viwanja hivyo.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi , wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja, wakati akitembelea banda la maoneshe la Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, yanayofanyika katika viwanja vya maonesho vya Nyamanzi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 14-4-2024.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, wakimsikiliza Afisa Masoko na Uhusiano wa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) Asha Kassim Biwii,wakati akitembelea banda la maoneshe la (ZHSF) wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, yanayofanyika katika viwanja vya maonesho vya Nyamanzi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 14-4-2024.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi, akimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Fatma Mabrouk Khamis ,wakati akitembelea banda la maonesho la Wizara hiyo katika viwanja vya Maonesho Nyamanzi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi “B”, Unguja, wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi, akimsikiliza Mkurugenzi wa (BOT) Tawi la Zanzibar Camillus Kombe,wakati akitembelea banda la maonesho la (BOT) katika viwanja vya Maonesho Nyamanzi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi “B”, wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi na (kulia kwa Rais) Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla,wakimsikiliza Katibu Msaidizi wa Tume ya Pamoja ya Fedha (JFC) Jonas Nduttu, wakati akitembelea banda la maoneshe la (JFC) wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
WASANII wa Kikundi cha Ngoma ya Kiumbizi  kutoka Pembe Kijiji cha Pujini wakitowa burudani ya wakati wa Uzinduzi wa Maadhimishio ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uliofanyika katika viwanja vya Moanesho Nyamanzi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi "B" Unguja leo 14-4-2024.

Na Mwandishi wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye nyanja zote za maendeleo, kisiasa, Uchumi, utamaduni na huduma za jamii yameipatia nchi heshima kubwa kwenye Jumuiya ya Kimataifa.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo viwanja vya maonesho ya biashara Nyamanzi Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magaharibi wakati wa uzinduzi wa Sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema, kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano huo, Tanzania imeendelea kubaki kwenye historia na mfano bora wa kudumisha Muungano barani Afrika na duniani kote kutokana na misingi thabiti ya umoja, amani na mshikamano viliyoasisiwa na viongozi Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na viongozi wenzao waasisi wa Muungano huo.

“Tunaposherekea miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, tuna wajibu wa kujipongeza kwa mafanikio makubwa nchi yetu iliyoyafikia kwenye nyanja zote za maendeleo kisiasa, kiuchumi na huduma za jamii. Alisifu Dk. Mwinyi.

Alieleza dhamira ya dhati kwa viongozi mbalimbali walioshika nyadhifa za uongozi kwa awamu tofauti kwa Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendeleza maono ya Waasisi wa Taifa hili kumefanikisha kudumisha na kuimarisha Muungano huo.

“Tunafurahia kuona umoja wa Watanzania unazidi kuimarika, ushirikiano baina yetu kwa shughuli mbalimbali za maendeleo umeongezeka na amani ya nchi yetu inaendelea kudumu” Alisifu Rais Dk. Mwinyi.

Akizungumzia changamoto za Muungano, Rais Dk. Mwinyi alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeendelea kuchukua hatua madhubuti kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote za Muungano huo, ikiwemo kuunda Tume na Kamati kwa ajili ya kushughulikia hoja za Muungano.

Alisema, miongoni mwa Tume na Kamati hizo ni pamoja na Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Kushughulikia Masuala ya Muungano iliyoundwa mwaka 2006.

Alisema tangu mwaka huo hadi mwaka huu wa 2024, hoja 25 zilipokelewa na kujadiliwa, kati ya hoja hizo alieleza hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.

Aidha, hoja zilizobaki Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa zipo kwenye hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi.
 
Dk. Mwinyi pia alieleza Imani yake na kwa utashi wa dhamira ya dhati ya Serikali za pande zote mbili kwamba hoja zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi.

“Ni wajibu wetu sote kuulinda, kuendeleza, kuudumisha na kuimarisha zaidi ili tuzidi kunufaika sisi tuliopo leo pamoja na vizazi vyetu kwa dhamira ile ile ya Waasisi wa Taifa letu” Alisihi Rais Dk. Mwinyi.

Alieleza ndani ya kipindi miaka mitatu (2021 -2024) hoja 15 pia zilipatiwa ufumbuzi, kati ya hoja 18 zilizokuwepo.

Alisema, utatuzi wa changamoto za Muungano, umeongeza imani ya Watanzania kwa Serikali zote mbili za SMZ na SMT kwa kuimarisha na kudumisha amani ya muda mrefu na utulivu uliopo ambao ni Tunu muhimu na fahari ya Tanzania

Hata, hivyo Rais Dk. Mwinyi alitoa shukrani zake za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha Muungano na kuwa ni moja ya vipaumbele vyake.

Sambamba na kuwahakikishia Watanzania wote kwamba Serikali za SMZ na SMT zitaendelea kuchukua hatua ili taifa la Tanzania liendelee kusonga mbele kwa maendeleo na kuendelea kubaki kuwa nchi ya amani na utulivu.

Rais Dk. Mwinyi pia alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wenziwe na Wananchi wote wa Tanzania kuendelea kuulinda Muungano huo ili waendelee kuishi kwa amani na kuzidi kujiletea maendeleo binafsi na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla aliwashukuru Rais Dk. Mwinyi na Dk. Samia kwa namna wanavyoliongoza taifa kwa misingi ya kusimamia Muungano.

Aidha, umuhimu wa kuendelea kulindwa Muungano kuenziwa, kuimarishwa na kulindwa kwa maslahi ya Watanzania.

Alieleza, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Ofisi ya Muungano na Mazingira ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wanawajibu wa kuielewaja jamii juu ya historia ya Muungano kwa vizazi viliopo sambamba na kuwasihi Watanzania kuendelea kuu Watanzania.

Mapema akizungmza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dk. Selemani Saidi Jafo alisema historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeundwa na sababu nyingi hadi kufikia kusainiwa kwa hati ya Muungano mwaka 1964 chini ya waasisi wake Hayati baba wa Taifa Julius K. Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Akitaja baadhi ya sababu hizo zikiwemo urafiki na udugu wa damu wa Wananchi wa pande mbili za Muungano, lugha ya Kiswahili iliyowaunganisha watu wa pande mbili hizo, pamoja vyama vya ukombozi vya TANU na ASSP Waziri Jafo alieleza kwamba vilitoa mchango mkubwa kwenye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema katika kusheherekea Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wanatarajia kuzindua kitabu maalum kinachoeleza historia ya Muungano wa Tanzania kwaajili ya kufundishiwa Skuli za Sekondari nchi nzima.

Uzinduzi wa sherehe za miaka 60 ya Muungano wa Tanzania na Ufunguzi wa Maonesho maalum ya Taasisi za Muungano chini ya kaulimbiu, “Tumeshikamana na Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa Letu”, unaashiria kuanza rasmi kwa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo upandaji wa miti, usafi wa mazingira na ushiriki wa wananchi na viongozi kwenye matukio ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi kwa maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Pia uzinduzi huo unaashiria hatua za maendeleo kwenye upatikanaji wa fursa kwa Taasisi za Muungano na zisizo za Muungano, Makampuni na wajasiriamali ili kuionesha jamii huduma na bidhaa mbalimbali zinazopatikana katika shughuli zao.

Kilele cha sherehe hizo ni tarehe 26 Aprili, 2024 kwenye viwanja vya Uhuru, Dar es Salaam ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Posted by MROKI On Sunday, April 14, 2024 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo